Mada ya utume (umisheni) haijapewa mkazo na uzingativu upasao katika makanisa yetu ya mijini. Baada ya kuonekana kwa kiasi kikubwa kama kazi ya kuvuka bahari kwenda pembe za mbali za dunia, tumeshindwa kuipa uchambuzi wa kina na muhimu ambao inastahili. Kwa mtazamo wa upande mmoja, ukamilifu wa imani ya Kikristo unaweza kuonekana kama mwitikio wa utume, wito wa kwenda kwa mataifa na kumtangaza Yesu wa Nazareti kama Bwana na Mfalme wa utawala wa Mungu. Agano Jipya ni mkusanyo wa hati za kimishenari zilizotolewa kwa makanisa ambayo yalianzishwa na mitume, wamishenari wa awali wa imani ya Kikristo. Mungu mwenyewe ndiye mmishenari wa asili, aliyekuja ulimwenguni kwa njia ya Kristo na kuupatanisha ulimwengu na nafsi yake (2Kor. 5:18-21). Hakika, Ukristo ni utume.
Katika moduli hii muhimu tunachunguza mitazamo mbalimbali ya kibiblia ya utume na watu wa Mungu, kuanzia na mtazamo wa Utume kama Tamthilia, kama Mapenzi, na kama Vita. Kila moja ya picha au taswira hizi za kibiblia inatoa ufahamu juu ya tabia ya ahadi ya agano la Mungu na utendaji wake katika nyakati au sehemu mbalimbali za wakati ili kuleta ukombozi katika Kristo. Pia tunachunguza mada mbili muhimu zinazohusiana hasa na utume katika miji, maono ya Biblia ya huduma katika miji na kwa maskini. Tangu mwanzo, Mungu ameiagiza jumuiya yake ya agano kuishi kwa uaminifu katika agano la Bwana ili kwamba haki ije katika mji, na umaskini uondolewe na badala yake haki na uadilifu vitawale.