Utambulisho wa Yesu wa Nazareti na kazi yake bila shaka ni somo muhimu zaidi katika tafakari na huduma zote za Kikristo. Ni ukweli usiopingika kwamba haiwezekani kuhudumu katika Jina la Bwana Yesu Kristo ikiwa huduma hiyo imejengwa juu ya maoni na mitazamo potofu na ya aibu kuhusu yeye alikuwa nani (na ni nani), maisha yake yalimaanisha nini, na vile tunavyopaswa kumchukulia leo. Kuwa na ufahamu sahihi juu ya maisha yake, kifo chake, ufufuo wake, kupaa kwake, na kurudi kwake ndio msingi wa kila kitu kwetu. Moduli hii inaangazia maisha na matendo yake makuu, na kuwa na umahiri katika maarifa ya kibiblia kuhusu yeye ndio jukumu hasa la ufuasi na huduma yoyote makini, ya kweli na yenye ufanisi.
Katika kozi hii muhimu, kwanza tunazingatia umuhimu wa Tamko la Imani la Nikea kwa masomo ya Kikristo, hasa jinsi linavyoweka kazi ya Kristo katika mitazamo miwili: kunyenyekezwa kwake (yaani, kufanyika kwake mwanadamu na kufa msalabani kwa ajili yetu) na kuinuliwa kwake (kufufuka kwake, kupaa kwake, na tumaini la kurudi kwake katika nguvu). Tutaangalia ubinadamu wa Kristo na mwelekeo wake wa pande mbili: kutufunulia utukufu wa Baba na kutukomboa kutoka katika dhambi na nguvu za Shetani. Tutachunguza uzushi muhimu unaotilia shaka asili yake ya kibinadamu, na kuchunguza matokeo ya kitheolojia ya kunyenyekezwa kwa Yesu na kifo chake, na nadharia mbalimbali za upatanisho ambazo zimetafuta kueleza maana ya kifo chake kwa ajili ya wanadamu. Hatimaye, tutazingatia vipengele vya matukio mawili ambayo yanaashiria kuinuliwa kwa Kristo, yaani, ufufuo wake na kupaa kwake kwa Baba. Tutamalizia somo letu kwa kutazama kuja kwake katika utukufu, hukumu yake kwa mataifa, na utawala wake ujao akiwa Mfalme katika Ufalme wa Mungu.