product.title

Module 1: Uongofu na Wito

Bila shaka, nyenzo ya kiroho yenye nguvu zaidi katika Kanisa ni Neno la Mungu lililovuviwa na Roho Mtakatifu, Maandiko Matakatifu. Kama wanafunzi wa Yesu Kristo, tunathibitisha imani yetu ya kina juu ya nguvu za Neno la Mungu katika kuumba, kuthibitisha, kugeuza na kuita. Ili kuelewa baraka ya ajabu ya uongofu na wito, tutahitaji kutathmini kwa kina nafasi ya Neno la Mungu katika Kanisa.

Moduli hii inaangazia nguvu ya Neno la Mungu kuwageuza waliopotea na kuwalinda walioitwa katika mapenzi kamili ya Mungu. Tunaanza na mjadala wa jinsi Biblia inavyojifafanua yenyewe kuwa ni Neno lenyewe la Mungu, lililovuviwa na “pumzi ya Mungu,” Roho Mtakatifu. Kupitia huduma yake kwa njia ya Maandiko Matakatifu, tunaelewa kwamba Neno la Mungu lina fungu muhimu katika kuzaliwa upya kwa mtu aliyepotea; kwa Neno, Roho huuthibitishia ulimwengu kwa habari ya dhambi, haki, na hukumu. Neno la Mungu hutugeuza; ni Neno linaloleta maisha mapya, na ambalo kwa lugha nyingine ni Injili ya Yesu. Ni Neno ambalo hutufanya “kuzaliwa mara ya pili,” kupata uzoefu wa kuoshwa kwa kuzaliwa upya, na kufanywa upya na Roho Mtakatifu, likizalisha ndani ya wale wanaoamini ishara halisi za nguvu ya Mungu ya kufanya upya. Hatimaye, tunaona jinsi Neno hili linavyotuita kutoka gizani kuingia katika maisha mapya katika Kristo. Tunachunguza dhana ya (metanoia), yaani, toba kwa Mungu, na imani (pistis). Neno la Mungu huzaa imani katika Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi ambaye anaokoa na kumkomboa mwamini kutokana na adhabu, nguvu, na uwepo wa dhambi.